Mwanasheria Mkuu wa TBS Afikishwa Mahakamani

Mwanasheria Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Baptister Marco (54) amepandishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka matatu ya kuishi na kufanya kazi nchini bila kuwa na  kibali.

Mwendesha Mashtaka wa Uhamiaji, Novatus Mlay alimemsomea mashtaka hayo leo Jumatano kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa.

Akisoma hati ya mashtaka,  Mlay alidai kuwa  Mei 19, 2017  huko Kinondoni katika ofisi ya uhamiaji,  Marco akiwa raia wa Burundi alikutwa nchini bila kuwa na kibali cha kumuwezesha kuishi.

Marco katika shtaka la pili amedaiwa kuwa siku hiyo alikutwa akifanya kazi kama Mwanasheria Mkuu wa TBS bila ya kuwa na kibali kinachomruhusu kufanya kazi hapa nchini.

Katika shtaka la tatu, Mlay alidai kuwa, Julai 6 mwaka 2011 katika ofisi ya Uhamiaji ya Dar es Salaam iliyopo Wilaya ya Ilala, mshtakiwa huyo akiwa raia wa Burundi alitoa taarifa za uongo kuhusu maelezo yake binafsi wakati akijaza fomu ya kuomba hati ya kusafiria namba CT (5)(Ai).

Wakili Mlay alisema kitendo hicho cha kutoa taarifa za uongo kilimuwezesha Marco kupata hati ya kusafiria ya Tanzania yenye namba AB 474856 huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, alikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Mshtakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh 20 milioni na alikamilisha. Kesi imeahirishwa hadi Juni 21, 2017 kwa ajili ya kutajwa.

Waziri Mkuu Majaliwa apokea taarifa ya mgogoro wa Loliondo....

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea Taarifa ya Kamati Shirikishi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ya kushughulikia mgogoro wa matumizi ya ardhi kwenye pori tengefu la Loliondo mkoani Arusha, ambapo atatoa maelekezo baada ya kuisoma.

Alipokea taarifa hiyo juzi katika kikao alichokiitisha kwenye ukumbi wa Spika, Bungeni mjini Dodoma. Waziri Mkuu aliiunda kamati hiyo, Desemba mwaka jana mara baada ya kumaliza ziara ya kikazi mkoani Arusha.

Kiini cha mgogoro huo ni eneo la pori tengefu la Loliondo ambalo linagombewa na wawekezaji, wakulima, wawindaji kwa sababu ni mapitio ya wanyama, chanzo cha maji, mazalia ya wanyama, malisho ya mifugo na makazi.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Tate William Ole-Nasha, viongozi wa mkoa wa Arusha na wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii. Wengine ni Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Rashid Taka, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa wa Arusha na wilaya ya Ngorongoro, wawakilishi wa wananchi, wawekezaji na asasi za kiraia ambao wote walishiriki katika uandaaji wa taarifa hiyo.

Waziri Mkuu alisema lengo la kamati hiyo ni kutaka kupata muafaka wa matumizi ya rasilimali zilizoko katika eneo hilo ili kila upande uweze kutekeleza majukumu yake bila ya kuathiri mwingine na kuwezesha wananchi wote kunufaika na rasilimali zilizoko katika eneo hilo.

“Serikali inataka watu wote tuwe kitu kimoja katika kutunza maeneo yetu, lakini pia shughuli za wananchi nazo ziweze kuendelea ili Watanzania wote tuweze kunufaika na rasilimali zilizoko kwenye maeneo yetu,” alisema.

Mfanyabiashara Auawa kwa Risasi Singida.. Soma Hapa

Mauaji ya kutumia silaha za moto yameendelea kushamiri nchini,baada ya mfanyabiashara mmoja mjini Singida kufariki dunia baada ya kupigwa risasi ya bunduki aina ya bastola wakati akitaka kuondoka dukani kurejea nyumbani.

Mfanyabiashara huyo na mkazi wa Itungukia tarafa ya Mungumaji manispaa Singida ni Simon Charles (49).

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa jeshai la polisi mkoa wa Singida,ACP Debora Magiligimba, alisema tukio hilo la kusikitisha limetokea Aprili, 20 mwaka huu saa 3.30 usiku.

Alisema siku ya tukio baada ya mfanyabiashara huyo kufunga duka lake la madawa ya binadamu lililopo standi ya zamani ya mabasi alianza kuelekea kwenye gari lake ili aweze kurejea nyumbani kwake.

“Wakati akikaribia gari lake ghafla muuaji huyo ambaye alijificha upande mwingine wa gari hilo alinyanyuka na kumpiga risasi titi la upande wa kulia na kutokea nyuma na kisha kudondoka pale pale. Wasamaria wema waliweza kumkimbiza hospitali ya mkoa lakini alifariki akipatiwa matibabu.Kifo chake kinatokana na kuvuja damu nyingi,” alisema Magiligimba. 
Kamanda huyo alisema kwenye eneo la tukio kulipatikana ganda moja la risasi ya bastola. Hadi sasa chanzo cha mauaji hayo, bado hakijajulikana.

Katika hatua nyingine, Magiligimba alisema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali kubaini watu waliojihusisha na tukio hilo ili waweze kukamatwa na sheria ziweze kuchukua mkondo wake.

“Jeshi la polisi linatoa wito kwa wananchi wote mkoani kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kusaidia kukamatwa kwa wauaji hao. Pia wafanyabiashara tunawakumbusha umuhimu wa kuajiri walinzi, watakaowalinda wao na mali zao,” alisisitiza.

Habari kutoka eneo la tukio, zinaeleza kwamba mfanyabiashara huyo ambaye kitaaluma ni daktari wa binadamu ameauwa na mtu mmoja ambaye alivalia suruali. Baada ya mauaji hayo, mtu huyo aliondoka kwa miguu na kutokomea kusiko julikana.

Mashuhuda wengine wanadai kuwa muuaji huyo hakuweza kukamatwa wala kufukuzwa, kwa madai kuwa mlio wa risasi ya bastola haukuwa mkubwa hivyo wakahisi kuwa ni tairi la pikipiki limepasuka na hivyo walipuuzia.

Chanzo: Modewji
© Copyright Nipashe Blog Published.. Blogger Templates
Back To Top